SHINDANO LA UANDISHI WA INSHA

Uandishi ni nguzo muhimu katika ufunzaji wa lugha. Ujuzi wa uandishi umechangia pakubwa kwa waelekezi kuweza kueneza lugha mbalimbali na kufanikisha mawasiliano kwa watu wengi katika maeneo mbalimbali. Wanafunzi wengi hukosa kufanya mazoezi ya kuandika na kama njia moja ya kuwapa motisha, niliwahimiza (Evans Mosoti) washiriki katika shindano la uandishi wa insha.

Gazeti la Taifa Leo limekuwa likiandaa shindano la insha kila mwezi. Shindano hili huhusisha wanafunzi kutoka shule mbalimbali kote nchini ambao huwa katika maeneo saba. Majina ya washindi kumi bora kutoka kila eneo huchapishwa kwa gazeti huku mshindi akituzwa baada ya kila mwezi. Shindano kuu la kujishindia karo litakalowashirikisha washindi wa kila mwezi, litaandaliwa mara moja pekee mwishoni mwa mwaka.

Mwezi wa Mei, wanafunzi wawili waliweza kuibuka kati ya kumi bora, na mmoja wao kuchukua nafasi ya kwanza katika eneo la Nairobi. Job Mugane, aliyekuwa bingwa wa eneo la Nairobi, alipata fursa ya kuzuru jumba la ‘Nation’. Aliweza kukutana na afisa mkuu mtendaji aliyempongeza na vilevile mhariri wa Taifa Leo aliyemkabidhi hundi. Isitoshe, alipewa ziara fupi ya studio za NTV, QTV na Nation FM.

Shindano la mwezi wa Juni lilichangamkiwa na wanafunzi wengi. Matokeo yaliyochapishwa yalikuwa na wanafunzi sita wa Strathmore kati ya kumi bora eneo la Nairobi. Wanafunzi wamejitolea na tunatarajia kufanya vyema katika miezi iliyobaki inshallah.
Kiswahili kitukuzwe.

Support our bursary fund!